-->

Thursday, February 8, 2018

MAKABIDHIANO YA NYUMBA ZA MAKAZI IYUMBU KATI YA NHC NA UHAMIAJI
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limekabidhi nyumba za makazi mnamo Tarehe: 24 Januari, 2018 zilizojengwa kwenye mradi wa kitovu cha mji wa kisasa wa nyumba za gharama nafuu wa Iyumbu Satellite Centre kwa Idara ya Uhamiaji.

Mradi huu ambao ujenzi wake ulianza Desemba 2016 una ukubwa wa ekari 234 na ni moja ya sehemu ya mji uliopangiliwa kitaalamu kwa kuzingatia sheria na kanuni za mipango miji na utajengwa katika awamu tatu. Nyumba hizi 63 ambazo zimeshakamilika na kuanza kukaliwa zinakabidhiwa leo kwa Idara ya Uhamiaji.
 
Makabidhiano haya yamefanywa na Meneja Masoko wa Shirika la Nyumba la Taifa, Ndugu Itandula Gambalagi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NHC na Kamishna wa Fedha, Ndugu Peter Chogero kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Uhamiaji.

Makabidhiano haya yanafanyika baada ya ahadi ya Shirika la Nyumba kwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ya kujenga nyumba makao makuu ya nchi Dodoma.
Katika uzinduzi wa nyumba hizi mwezi disemba 2017, Mkurugenzi Mkuu wa NHC alimhakikishia Mh. Rais kwamba nyumba hizi zimekamilika na ziko tayari kwa kukaliwa.
 
Ni furaha kuona kwamba NHC inakabidhi nyumba kwa Uhamiaji ambaye ni mmoja wa wanunuzi wakubwa wa nyumba katika mradi huu.
Nyumba hizi ni bora kabisa zimejengwa kwa ustadi mkubwa. Ni wito wetu kwamba nyumba hizi watazitunza ikiwa na mazingira yake.
Mradi huu wa nyumba 300 ikiwa 150 zimekamilika ni kati ya miradi mingi ambayo NHC inatekeleza.
Tunatoa mwito kwa wateja wote waliomaliza kulipa wajiandae kukabidhiwa nyumba zao, na wale ambao hawajamaliza malipo wafanye hivyo haraka ili wakabidhiwe nyumba zao.
Tunatoa pongezi kwa wadau wetu Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Mamlaka ya Maji Safi DUWASA, Tanesco, Tanroad, Jeshi la Polisi kwa ushirikiano mkubwa katika kuufanya mji huu wa Iyumbu ukamilike.
Na mwisho niwaombe tena Uhamiaji waendelee kutuunga mkono katika juhudi zetu za ujenzi wa nyumba na isiwe mwisho kununua nyumba NHC.